UTANGULIZI.
Mheshimiwa makamu wa Rais, Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshiwa Katibu wa Bunge, Mheshimiwa Katibu Mkuu kiongozi wa serikali ya wanafunzi, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bunge, Waheshimiwa kutoka ofisi ya Waadili, Waheshimiwa Mawaziri, Ma naibu waziri pamoja na Makatibu wakuu wa wizara, Waheshimiwa Wabunge wa baraza hili tukufu la wawakilishi MWECAUSO, ndugu wageni waalikwa na wote mlio shiriki katika mkutano huu mkubwa wa bunge itifaki ikiwa imezingatiwa, habarini za muda huu.
SHUKRANI
Mheshimiwa Naibu Spika,
Awali ya yote, nichukue fursa hii kwa unyenyekevu mkubwa kumshukuru Mwenyezi MUNGU muumba wa mbingu na dunia kwa zawadi ya uhai na kwa namna ambavyo ametujaalia na ameendelea kutujalia Afya njema, Furaha, Amani, Hekima, Busara za kiungozi ,Ushirikiano, Maarifa, Nidhamu na Upeo wa kuweza kuyatimiza yote tuliyo yatimiza katika kipindi hiki cha uongozi wetu. Itoshe kusema MUNGU ni mwema kwa watu wake na hakika amekua mwema kwetu, sambamba na hilo nitumie fursa hii kuwakumbuka na kuwaombea wanafunzi wenzetu waliotangulia mbele ya haki ambao ni Ndugu SYLIVESTER RAMADHAN ALLY na Ndugu ADAM ADEN, MUNGU awapumzishe katika ufalme wake kwa Amani na awaangazie mwanga wa milele. AMINA.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Moyo usio na shukrani hukausha mema na wema wote; nitumie nafasi hii kuishukuru menejimenti ya Chuo chetu kikuu cha Kikatoliki Mwenge chini ya uongozi makini na mahiri wa makamu mkuu wa chuo Profesa PHILIBERT VUMILIA pamoja na wasaidizi wake profesa HENDRY LASWAI ( DVCAA) na padre daktari EUGENE LYAMTANE (DVCAF) kwa ushirikiano wao mkubwa walio tuonyesha kwenye kipindi chote cha uongozi wetu kwa kuishauri, kujibu na kutatua kero na mapendekezo ya wana MWECAU kwa haraka na kwa wakati. Kwa moyo wa dhati na wa kipekee kabisa, nimshukuru mwadili wa wanafunzi padre. Placido Mwanyika na wasaidizi wake ndg. Florence Haule na mama yetu Editha Rambau kwa namna ambavyo wameendelea na wanaendelea kuwa msaada kwa wanafunzi wenzetu na kwetu sisi kama serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Pia nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Spika Ndugu JACKSON MKALAWA kwa namna ambavyo amekuwa akiliongoza bunge hili kwa weledi mkubwa na kunipa kibali cha kuja kulihutubia bunge hili mara kadhaa. Aidha nikushukuru wewe Naibu Spika, Mheshimiwa Angela Jerome kwa weledi mkubwa, ujasiri,uwezo na kuwa mfano kiutendaji katika ofisi ya spika kwa namna ambavyo umekuwa ukizisimamia shughuli mbalimbali za bunge. Pia, nimshukuru katibu wa bunge Mheshimiwa Masaka Daniel Salum pamoja na mwenyekiti wa bunge Mheshimiwa John Martin Kwa ushirikiano mzuri uliokuwepo kati ya mihimili yetu miwili katika kipindi chote cha uongozi wetu tangu tarehe 03/08/2019. Vilevile ninawashukuru waheshimiwa wabunge wa bunge lako tukufu la MWECAUSO kwa ushirikiano wao wa dhati kabisa katika kutekeleza wajibu wao wa kuwatumikia wanafunzi wa chuo kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Niseme wazi kuwa bunge hili limekuwa la kitofauti na lenye watu makini kwani pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali waheshimiwa mawaziri, manaibu waziri, makatibu wa wizara na wabunge wameonyesha ushirikiano mkubwa katika kutimiza majukumu na shughuli mbalimbali za ujenzi wa serikali yetu na chuo kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Mnamo tarehe 03/08/2019 nilikuja hapa kulizindua bunge hili tukufu la MWECAUSO 2019/2020. Leo tena kwa madhumuni ya kutimiza matakwa ya katiba yetu nimekuja kulihutubuia kwa mara ya mwisho ili hatimaye kuweza kuruhusu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge katika Chuo chetu Kikuu cha Kikatoliki Mwenge baada ya kupitishwa kwa tume ya uchaguzi unao tarajiwa kufanyika tarehe 12/07/2020; Siku nazindua bunge hili nakumbuka nilieleza mambo mengi sana ambayo nafarijika kuona kua mengi tumefanikiwa kuyatekeleza kama vile ambavyo waheshimiwa mawaziri walieleza katika uwasilishaji wa ripoti zao za wizara, aidha bunge lililopita mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelezo ya kina kuhusu mafanikio yaliyopatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Kwa ujumla naweza kusema katika kipindi cha serikali yetu ya awamu ya 19 tumeweza kutimiza wajibu wetu wa kuwatumikia wana MWECAU kwa kiasi kikubwa; Aidha tumeweza kufanya hivyo kutokana na ushirikiano mkubwa tulioupata kutoka kwa wana MWECAU wote, hivyo nitumie fursa hii kwa mara nyingine kuwashukuru ninyi waheshimiwa wabunge kwa kuishauri vyema na pia kuisimamia vizuri serikali katika kutekeleza majukumu yake. Aidha nawashukuru waheshimiwa wawakilishi wa madarasa kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa shuguli mbalimbali za kitaaluma kwenye madarasa yao kama sehemu ya kutimiza wajibu wao kiserikali. Kama tunavyo fahamu wawakilishi wa madarasa ni viungio muhimu kati ya wana MWECAU na serikali, na pia kati yenu waheshimiwa wabunge na wanafunzi. Hivyo hatuna budi kuwashukuru wawakilishi wetu wa madarasa.
Napenda pia nitumie fursa hii kuwashukuru watangulizi wangu katika awamu tofauti tofauti kwa kuweka misingi imara na kutengeneza mazingira yaliyowezesha kupatikana mafanikio haya mbalimbali katika kipindi cha ungozi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Kama tunavyo kumbuka, moja wapo ya ahadi na ombi kubwa nililo litoa wakati wa kuzindua bunge hili tukufu ilikuwa ni kudumisha Amani, umoja, uelewano na ushirikiano kati ya mihimili yetu miwili ya MWECAUSO na kuepuka mafarakano yaliyokuwapo wakati ule ambapo niliyataja kama ‘panya na paka’. Ninayo furaha kulitaarifu bunge lako tukufu kwamba sisi sote tumetimiza ahadi hiyo kwa vitendo, wana MWECAU tumebaki kuwa wamoja na tumeendelea kushirikiana katika mambo mengi licha ya tofauti zetu kivitiivo, kirangi, kikabila na kiuwezo wetu binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Nitumie fursa hii kulikumbusha bunge lako tukufu kwa ufupi kabisa juu ya yale mambo ambayo serikali ya awamu hii 2019/2020 iliahidi kuyafanya katika kipindi chake cha uongozi
Mheshimiwa Naibu Spika,
Utakuwa shahidi mzuri wa bunge lako tukufu juu ya mambo mengi ya kiutendaji na kiutekelezaji ambayo niliahidi kupitia ilani yangu ya uchaguzi yakiwa katika mgawanyo wa wizara mbalimbali kwa mujibu wa katiba yetu toleo la 2018. Naomba kulitaarifu bunge lako tukufu na wana MWECAU wote kwa moyo wa ujasiri na kujiamini kuwa yote niliyoyaahidi katika ilani yangu katika wizara mbalimbali yametekelezeka kwa zaidi ya asilimia 96%. Na hapa nitayataja baadhi ya mambo machache katika mengi ambayo yametekelezwa na serikali ya wanafunzi ya chuo kikuu cha Kikatoliki Mwenge awamu ya 19 mwaka 2019/2020.
SEKTA YA ELIMU.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Kama serikali, tukitambua kuwa elimu ndiyo msingi wa sisi kuwepo hapa chuoni, tulijikita katika kuimarisha na kuboresha miundo mbinu ya kufundishia na kujifunzia kwa kuwasilisha hoja zetu kama serikali ndani ya utawala ambapo mambo mbalimbali yametekelezwa na menejimenti ya chuo ikiwemo matengenezo ya ‘projector’
Mheshimiwa Naibu Spika,
Katika ilani yangu niliahidi kuhakikisha uwepo wa feni ndani ya ukumbi wa Dr msaki ambapo ‘estate manager’ kwa kulitekeleza hili, aliweka ventilation ndani ya ukumbi ule kama mbadala wa feni. Naomba kulitaarifu bunge lako na umma wa wana MWECAU kwamba hili limetekelezwa kwa asilimia mia moja ili kuhakikisha mazingira rafiki ya kujifunzia hasa wakati wa kipindi cha joto. Lile lililofanyika pale ni awamu ya kwanza bado awamu ya pili ya utekelezaji wake itaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Sambamba na hilo kama serikali tumehakikisha uwekwaji wa ‘projector’ ndani ya madarasa ya kujifunzia yaliyokua hayana ‘projector’ kuanzia L8 hadi L23. Haya ni mafanikio makubwa kwa serikali na chuo chetu kwani, kwa njia hii taaluma katika chuo chetu itazidi kuwa imara na ni njia ya kuelekea ‘mission’ ya chuo chetu, chuo kikuu cha Kikatoliki Mwenge ambayo ni kuzalisha wahitimu bora, mahiri na wenye ushindani katika nyanja mbalimbali kama vile tafiti kikanda, kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Pamoja na marekebisho ya miundo mbinu ya kujifunzia kama vile vipaza sauti na projector katika madarasa mbalimbali hapa chuoni, pia mchakato wa matengenezo ya vimbweta uko mbioni na utakamilika siku za usoni ili kuweka mazingira rafiki ya majadiliano kipindi cha mithiani ambapo madarasa huwa yanafungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Serikali imefanikiwa kuboresha na kuimarisha uhusiano mzuri na wawakilishi wa madarasa kupitia wizara ya elimu kwa kufanya vikao vilivyo lenga kujadili changamoto wanazo kumbana nazo katika utendaji kazi wao. Kwa kutambua mchango wao na umuhimu mkubwa walionao katika serikali ya wanafunzi hapa chuoni, serikali iliamua kutenga zaidi ya asilimia 68 ya bajeti mama ya wizara ya elimu kwaajili ya wawakilishi wa madarasa ili kuwapa motisha zaidi katika utendaji kazi wao. Samabamba na hilo serikali imehakikisha mchakato wa utengenezaji wa vyeti kwa wawakilishi wa madarasa wanaohitimu pamoja na kuandaa mahafali yao. Na hii inakuwa ni mara ya pili kwa serikali hii kutunuku vyeti kwa wawakilishi wa madarasa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Wakati nazindua bunge hili, nilieleza kwa kirefu sana kuhusu nia na lengo la serikali ya MWECAUSO awamu ya 19 katika kukitangaza chuo, hivyo basi katika kipindi cha serikali yetu tumejitahidi kushugulikia suala hilo kwa kuhakikisha ushiriki wa wanafunzi wengi katika mashindano ya ‘Capital Market Security Autholity (CMSA), ambapo mwanafunzi mwenzetu ndugu ELIA WISTON alishika nafasi ya tatu katika shindano la uandishi wa makala ya juu ya masoko kitaifa, hivyo kukitangaza chuo chetu vizuri Katika ngazi ya taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Serikali kupitia mkuu wa idara ya biashara Dactari George Mkoma imekwisha kuweka mikakati kwamba pamoja na hiari ya mwanafunzi yeyote kushiriki, ni lazima wanafunzi wote wanaosoma masomo ya biashara hapa chuoni kushiriki katika mashindano hayo. (Ni lazima siyo hiari). Kwa manufaa mapana ya wanafunzi wenyewe na chuo chetu kwa ujumla. Sambamba na hilo serikali ya MWECAUSO 2019/2020 imefanikiwa kukitangaza chuo kwa kusambaza vipeperushi vya chuo chetu kwenye maeneo mbalimbali nchini katika ziara zote ambazo viongozi wa serikali wamefanya ndani ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Mheshimiwa spika ni shahidi katika ziara yetu ya kwanza ya ukaguzi wa miradi ya serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na mahafali ya wanafunzi bora vyuo vikuu kitaifa pamoja na mkutano na waziri mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 8 hadi hadi 11/8/2019 ambapo mambo mbalimbali yanayohusu vyuo na wanafunzi yalijadiliwa, tulifanikiwa kusambaza vipeperushi zaidi ya 200 kama moja ya hatua ya kukitangaza chuo chetu. Nimshukuru mbunge wa hosteli za wavulana Mheshimiwa Ndugu Severino Paul kwa ushiriki wake wa moja kwa moja katika hili, kwani alichukua vipeperushi zaidi ya 100 katika ofisi yangu na kwenda navyo wakati wa likizo kwaajili ya kukitangaza chuo chetu pendwa cha MWECAU katika mazingira aliyoenda.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Hii bila shaka inaonyesha dhamira yetu isiyo na mashaka kama serikali ya kukitangaza Chuo chetu Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Naupongeza mhimili wa bunge, serikali na wana MWECAU wote kwa ujumla kwa kufanikisha jambo hili.
SEKTA YA AFYA, CHAKULA, NA MAZINGIRA
Mheshimiwa Naibu Spika,
Kuhusu afya, chakula na mazingira, serikali imeendelea kuhakikisha zoezi la usafi wa mazingira kwa kila jumamosi ya mwisho wa mwezi linafanyika katika mazingira ya chuo chetu ikiwemo suala la upandaji na utunzaji wa miti kwa kushirikiana kwa ukaribu kabisa na klabu ya mazingira pamoja na afisa mazingira wa chuo chetu, utakumbuka kuwa katika wiki ya mazingira duniani nilisisitiza katika hotuba yangu ndani ya bunge la dharura juu ya umuhimu wa ushiriki wetu sote katika kilele cha maadhimisho hayo. Zaidi ya miti 60 ilipandwa kwa lengo la kuendelea kuweka mazingira yetu katika hali ya ubora. Sambamba na hilo kwa kushirikiana na ofisi ya ‘estate manager’ tumefanikiwa kuweka vitunza taka katika maeneo yote ya chuo kwa lengo la kuendelea kuweka mazingira yetu ya chuo katika hali ya usafi.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa COVID 19, serikali imefanikiwa kukaa vikao mbalimbali na ofisi ya waadili pamoja na menejimenti ya chuo na kuandika nyaraka tafouti tofauti za kuutarifu umma wa wana MWECAU kuhusu taarifa mbalimbali na taratibu za kujikinga na janga la COVID 19 kama chuo. Pia, waraka uliandikwa kwenda serikali ya kijiji kwa wamiliki wa nyumba kuhusu kusamehewa kodi kwa kipindi tulichokuwa likizo ya CORONA. Niwashukuru wamiliki wote wa nyumba waliopokea ombi letu kama serikali na kuwasamehe baadhi ya wana MWECAU. Miundo mbinu ya kutosha na inayo kidhi mahitaji imewekwa katika kupambana na janga la COVID 19 katika chuo chetu kama vile maji tiririka na vipima joto; nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru uongozi wa Chuo chetu Kikuu cha Kikatoliki Mwenge kwa namna ambavyo wamelichukulia kwa uzito janga hili la homa kali ya mapafu na kuweza kupambana na kufanikiwa kulidhibiti janga hili katika chuo chetu kwa kuweka miundo mbinu bora, imara na ya kudumu. Ni chuo chetu pekee kimeweza kuweka miundo mbinu imara na bora ya kutosheleza idadi kubwa ya wanafunzi kuliko chuo kingine chochote Tanzania ingawa hakukuwa na bajeti yake.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Katika kukabiliana na changamoto ya ucheleweshwaji wa bima za afya serikali kwa kushirikiana na ofisi za bima ya afya mkoa tumefanikiwa kuanzisha mfumo wa usajili wa bima za afya kwa njia ya TEHAMA ‘online system’ ambapo wanafunzi wote wamesajili bima zao kwa mfumo huu. Hii imeondoa changamoto ya kufungwa kwa mfumo wa kusajili vitambulisho vya bima uliokuwepo hapo awali kwani kwa sasa mwanafunzi anaweza kurejesha uhalali wa bima yake wakati wowote bila ukomo wa muda. Sambamba na hilo serikali ilifanikiwa kutoa semina kwa wanafunzi wote juu ya namna ya usajili wa bima kwa mfumo huu mpya kutoka kwa maafisa wa mfuko wa bima ya afya wa mkoa,
Hali kadhalika serikali imefanikiwa kuendesha zoezi la uchangiaji wa damu salama kwa vipindi tofauti tofauti na kuendesha zoezi la upimaji wa virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Nichukue fursa hii kuwashukuru wote walioshiriki katika zoezi la uchangiaji damu salama kwa vipindi tofauti tofauti na kwa namna ya kipekee kabisa niwapongeze waheshimiwa mawaziri, manaibu waziri, makatibu wa wizara, wabunge na wana MWECAU wote walioshiriki katika zoezi la kuchangia damu tarehe 16 Na 17 julai katika chuo chetu eneo la mdegree ambalo lilikuwa na kauli mbiu ya Rudisha tabasamu la mgonjwa kwa kumpa zawadi ya uhai kama ilivyo desturi yetu wana MWECAU. Niwaambie tu kwamba wote mliochangia damu mmerudisha tabasamu la watanzania wengi. Zaidi ya wana MWECAU mia nane ambao ni sawa na zaidi ya asilimia 21.05 ya wana MWECAU wote wameshiriki kikamilifu katika zoezi hilo. MUNGU awabariki wote.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Kama chuo tumebahatika kuwa na kituo cha afya ambacho pamoja na uchanga wake kimekuwa kikitoa huduma nzuri kwa wana MWECAU na jamii inayotuzunguka. Kama serikali ya awamu ya 19, tumefanikiwa kutoa mapendekezo ya ununuzi wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) ambayo itakuwa inatoa huduma kwa jamii nzima ya wana MWECAU na viunga vyake kwa kutumia yale malipo ya dharura kutoka fedha ya tahadhari yaani CAPITATION FEE ambayo ni kiasi cha TSH: 49,600/= jambo ambalo kama uongozi walilipokea kwa mikono miwili na kulitekeleza. Nitumie fursa hii kuupongeza na kuushukuru uongozi wa chuo hasa ofisi ya naibu makamu mkuu wa chuo, utawala na fedha (DVCAF) kwa ununuzi huu wa gari hii katika utoaji wa huduma ya afya. Aidha kama serikali tumefanikiwa kuushauri uongozi wa kituo cha afya kuhusu utoaji huduma wa duka la madawa la hospitali nyakati za usiku. Kwa sasa huduma zinapatikana masaa ishirini na manne.
Haya ni mafanikio makubwa katika kujali afya na maisha ya wana MWECAU.
SEKTA YA MICHEZO, HABARI, NA MAWASILIANO.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Sisi kama serikali kwa kutambua michezo ni afya, na ni muhimu vijana kujiunga na kushiriki katika michezo, tumefanya maboresho makubwa katika uwanja wa mpira wa pete, ili kuwawekea wana MWECAU wanaoshiriki mchezo huu mazingira bora na rafiki Zaidi. Vilevile kama serikali tumefanya manunuzi ya vifaa vya michezo ili kuongeza tija katika sekta hii. Ninamshukuru na kumpongeza mheshimiwa mbunge Omary H Omary kwa ushiriki wake wa moja kwa moja katika kuboresha sekta ya michezo kwa kutoa vifaa vya michezo ikiwemo mipira. Sambamba na hilo la kuimarisha miundo mbinu serikali imefanikiwa kuandaa mechi za kirafiki na vyuo mbalimbali kama vile makumira, KCMC, Chuo Kikuu cha Ushirika kwa lengo la kuimarisha timu zetu , kudumisha mshikamono baina ya chuo chetu cha kikatoliki Mwenge na vyuo hivyo pamoja na kukitangaza chuo chetu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Katika kupunguza mikusanyiko isiyo kuwa ya lazima katika mbao za kutolea taarifa, serikali ya awamu ya 19, imeanzisha MWECAUSO NEWSLETTER na MWECAUSO LIVE katika mitandao ya youtube, facebook, Instagram na twitter ambavyo hutoa taarifa mbalimbali kila wiki, kwa kuzingatia matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii kwa lengo la kusambaza taarifa kwa haraka hasa kwenye kipindi hiki cha janga la corona; tofauti kabisa na serikali nyingine kurasa hizi za kijamii zitarithishwa kwa serikali ijayo ili kuendelea kuwahabarisha wana MWECAU kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Kila mmoja wetu hapa ni shahidi juu ya mashindano ya MWECAUSO CUP yaliyoandaliwa na serikali ya awamu ya 19 ya mwaka 2019/2020 ambayo yameitikiwa na wana MWECAU kwa mwitikio mkubwa. Nichukue fursa hii kuendelea kuwasihi wana MWECAU kushiriki katika michezo hii na kuendelea kuchukua tahadhari za dhati kabisa dhidi ya janga la COVID 19 wawapo uwanjani kwa kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kwani serikali imenunua zaidi ya ndoo ishiriki kwaajili hiyo, kadhalika uzingatiaji wa kuvaa barakoa na umbali wa mita moja baina ya mtu na mtu ni muhimu;
Aidha serikali imekuwa ikiendelea kulipia visimbuzi vya AZAM TV na DSTV kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanapata habari mbalimbali zinazo endelea pote duniani hasa habari pendwa na vijana, habari za michezo. Kwa kutambua ukubwa na uzito wa MWECAUSO CUP, serikali imehakikisha uwepo wa viongozi mbalimbali wa serikali wakati wa fainali na utoaji wa zawadi akiwemo mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mheshimwa mama yetu mpendwa ANNA ELISHA MGHWIRA mazungumuzo yanaendelea na viongozi wengine wa serikali na makampuni ili kuendelea kuyapa uzito zaidi mashindano haya.
SEKTA YA ULINZI MAKAZI NA MAMBO YA NJE.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Kama serikali tukitambua kwamba Amani, Ulinzi na Usalama wa chuo na wana MWECAU ni jambo la msingi katika kufanikisha shughuli nyingine zote, tumeendelea kuhakikisah Amani na usalama vinatawala katika mazingira yetu na mipaka yake. Utakumbuka kuwa wakati tukiingia madarakani kulikuwepo na wimbi kubwa la wahalifu katika makazi ya chuo pamoja na vitendo vingine vya kiuhalifu. Hata hivyo kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na serikali awamu hii ikiwemo kuweka doria na lindo la usiku kwa kushirikiana na serikali ya kijiji, vitendo hivyo vimekomeshwa kwa kiasi kikubwa na mazingira yetu yapo salama. Katika kipindi cha serikali yetu tumejitahidi pia kuwawekea dhamana wanafunzi ambao wamekuwa wakifikishwa kituo cha polisi kwa nyakati tofauti tofauti kwa kuonewa au kwa makosa yao binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Usalama si nyakati za usiku tu; yapo matukio mengine hatarishi kwa uhai wa wana MWECAU kama vile mwendo kasi wa vyombo vya moto; na kwa kulitambua hili serikali imefanya vikao na wenyeviti wa vituo vyote vya bodaboda vinavyo zunguka chuo chetu kupitia mwenyekiti wa kijiji na kujadili masuala ya kiusalama hasa kupunguza mwendo kasi pindi wakiwa karibu na mazingira yanayo zunguka chuo. Matuta yameshaanza kuwekwa, ikiwa ni moja ya mkakati wa kupunguza mwendokasi na kuweka barabara hizi zinazo kizunguka chuo chetu salama zaidi. Nimshukuru makamu mkuu wa chuo kwa kuamua kuunga mkono juhudi hizi za uwekwaji wa matuta kama sehemu ya kuongeza usalama.
Aidha, kwenye upande wa mambo ya nje serikali imeimarisha ushirikiano na makampuni mbalimbali ikiwemo halotel walio dhamini bonanza katika viwanja vyetu, ushirikiano na vyuo vingine kwa kuwa na ziara mbalimbali ambapo mambo mbalimbali yamejadiliwa kwa manufaa mapana ya chuo chetu na wana MWECAU kwa ujumla. Kwa kuzingatia adha ya usafiri kutoka ushirika wa neema hadi geti la chuo, serikali yetu kwa kushirikaina na mwenyekiti wa kijiji kupitia wizara ya mambo ya nje imejipanga kwenda ofisi za SUMATRA ili kupata utaratibu sahihi wa huduma hiyo. Serikali inapendekeza kuwepo kwa huduma ya bajaji hadi geti la chuo.
SEKTA YA MIKOPO.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Wanafunzi wengi wa elimu ya juu katika chuo chochote wamekuwa wakitegemea mkopo wa serikali katika malipo ya ada na fedha za kujikimu wawapo chuoni. Serikali ya awamu ya 19 kwa kulitambua hili imefanikiwa kuwasaidia wanafunzi zaidi ya 40 walio kuwa wamekosa mkopo wa serikali wakiwemo wanafunzi wa ‘project planning and management’ ambapo ilimlazimu hata waziri wa mkopo mheshimiwa SALUM ALEX kuliwasilisha katika kikao cha TAHLISO huku afisa mikopo akienda mara kwa mara bodi ya mikopo, kwa hili naipongeza wizara na afisa mikopo wa chuo chetu kwa kazi kubwa walio ifanya katika kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Kutokana na unyeti wa masuala ya fedha serikali ilifanikiwa kuandaa semina elekezi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya masuala ya mkopo, aidha serikali imehakikisha wanafunzi wanalipwa kwa wakati fedha zao za kujikimu kwa haraka iwezekanavyo hadi ndani ya siku tatu mara tu baada ya kusaini malipo yao ukilinganisha na utaratibu wa hapo awali ambao ulichukua hadi siku kumi na nne.
SEKTA YA KATIBA SHERIA, JINSIA NA USURUHISHI.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Kwa upande wa sekta ya katiba, sheria, jinsia na usuluhishi, kwa kushirikiana na uongozi wa chuo tumefanikiwa kuweka bango linaloonesha aina ya mavazi na vitu ambavyo haviruhusiwi ndani ya chuo chetu kwa kuzingatia maadili ya chuo chetu kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Hii imepunguza migogoro kati ya wanafunzi na walinzi ukilinganisha na hapo awali. Lakin pia serikali imegawa vitabu vya sheria ndogondogo zaidi ya 1200 kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza ili kuwapa wanafunzi uelewa wa sheria na taratibu za chuo na kuepuka uvunjifu wa sheria usio kuwa wa lazima au utokanao na kutokujua sharia.
SEKTA YA STAREHE NA MAAFA.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Katika sekta ya starehe na maafa kwa mara ya kwanza katika historia ya MWECAUSO, serikali imefanikiwa kuratibu tukio la kuwakaribisha mwaka wa kwanza na kuiingizia serikali mapato ya zaidi ya shilingi elfu tisini, tumezoea tukio hili ni tukio la kutumia fedha, kwa namna ya kipekee kabisa niipongeze wizara hii na kamati ya kudumu ya bunge ya wizara hii kwa kazi nzuri na ya kuigwa waliyoifanya; Aidha katika upande wa maafa serikali imeratibu mchango wa zaidi ya shilingi milioni tatu kwaajili ya kuwapa pole wanafunzi wenzetu walio potelewa na wazazi wao ikihusisha mchango wa pole kwa familia za wanafunzi wenzetu Sylivester Ramadhani Ally na Adam Aden walio poteza maisha katika kipindi cha serikali yetu.
SEKTA YA FEDHA NA MIPANGO.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Mwenendo wa taasisi yeyote unahitaji fedha, na, nikiri wazi kuwa wizara ya fedha na mipango imekuwa ikiendesha mambo kwa umakini wa hali ya juu sana, kwa kuwalipa kwa wakati viongozi wote wanao stahili kupatiwa malipo kwa misingi ya kikatiba na siyo kupeana peana tu. Hii imesaidia serikali kubana matumizi karibu kwa zaidi ya asilimia tano jambo ambalo ni mafanikio makubwa. Sambamba na hilo wizara ya fedha na mipango imefanikiwa kuiingizia serikali kiasi cha fedha zaidi ya milioni mbili kupitia mradi wa kamba ambayo imekuwa msaada mkubwa katika uendeshaji wa shughuli za serikali.
UTAWALA BORA.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Katika kipindi cha serikali yetu tumejitahidi kuimarisha maadili, nidhamu na utendaji kazi serikalini. Kama nilivyo ahidi kwamba hakutakuwa na mzaha kwa viongozi; na watumishi wazembe walio shindwa kufanya kazi kwa weledi, nidhamu, maarifa na uadilifu, viongozi wa namna hiyo walichukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo kupelekwa kwenye kamati ya maadili ya serikali na wakati mwingine kuwatumbua, jambo lililo leta ufanisi mkubwa katika utendaji wa serikali ya awamu ya 19 mwaka 2019/2020.
Aidha kwa ushirikiano na kwa upendo mkubwa wa menejimenti ya chuo tulifanikiwa kuongezewa ofisi tatu na hivyo kufanya Serikali ya wanafunzi hapa chuoni kuwa na jumla ya ofisi nne kwa lengo la kuongeza wigo na ufanisi wa kiutendaji. Sambamba na hayo uwajibikaji wa kila mmoja wetu kwa kujali utu, heshima, upendo na Amani kwetu sote wana MWECAU wakati wa utoaji wa huduma kumesaidia kuleta ufanisi kwa serikali yetu.
HITIMISHO.
Mheshimiwa Naibu Spika,
kwa kifupi sana haya ni baadhi tu ya mafanikio tuliyoyapata. Lakini Kama nilivyo sema awali kama serikali tumefanya mengi ambayo kama ningeamua kuyaeleza yote hapa tunaweza kukesha. Kwa bahati nzuri wana MWECAU wameyaona na wanayajua. Hivyo basi ninaimani wana MWECAU wataendelea kuchagua viongozi bora na imara kwa chuo chetu katika vipindi vingine ili kuendelea kukipatia chuo chetu maendeleo. Binafsi kutokana na misingi imara tuliyo iweka kama serikali ya awamu ya 19 na mafanikio makubwa tuliyo yapata, endapo wana MWECAU wataendelea kuchagua viongozi wazuri katika nyakati tofauti ni dhahiri wataweza kufanikiwa kutimiza ndoto na dhamira zao na kuifanya MWECAU na MWECAUSO kuwa mahali salama, pazuri pakuvutia na pendwa zaidi miongoni mwa vyuo vya mkoa wa Kilimanjaro na taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Pamoja na mafanikio yaliyo patikana zilijitokeza baadhi ya changamoto. Kama ujuavyo hapa duniani siyo rahisi kufanya jambo lisikumbane na changamoto ama vikwazo. Hivyo basi sisi pia katika serikali yetu ya tumekumbana na changamoto na vikwazo mbalimbali lakini kubwa zaidi ni janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu ambao kwa kiasi umeadhiri mwenendo wetu kimaisha hasa kwenye maisha yetu kielimu. Napenda nitumie fursa hii kulishukuru bunge hili tukufu kwa kupitisha bajeti mbalimbali za serikali lakini ukweli ni kwamba bajeti hizi hazikuwa za serikali bali za wana MWECAU wote ikiwa ni pamoja na bunge hili.
Nitumie fursa hii kwa mara nyingine kwa namna ya pekee kurudia kumshukuru Mwenyezi MUNGU kwa kuendelea kukilinda na kukiepusha Chuo chetu Kikuu cha Kikatoliki Mwenge dhidi ya ugonjwa wa corona; pia nilishukuru tena bunge lako tukufu kwa ushirikiano na uvumulivu wao pale changamoto zilipo jitokeza ikiwa ni pamoja na kuwasiliana moja kwa moja na ofisi ya Naibu Spika hasa kupitia katibu wa bunge mheshimiwa MASAKA SALUM MASAKA ambaye amekua msaada mkubwa na kiunganishi kizuri kati yetu, lakini pia miongoni mwa wabunge na kuangalia namna ya kuweza kutatua changamoto hizo katika mambo mbalimbali yahusuyo wanafunzi katika chuo chetu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
Mwanzoni mwa hotuba yangu nilieleza kuwa nimekuja kulihutubia bunge hili tukufu kwa mara ya mwisho ili kuruhusu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa serikali ya wanafunzi hapa chuoni. Nyote mnafahamu uchaguzi ni zoezi muhimu katika kukuza demokrasia mahala popote pale. Na katika hili, natambua kuwa baadhi yenu hapa mna nia ya kuwania tena nafasi mbalimbali za uongozi katika serikali hii kwa wale wenye vigezo kwa mujibu wa katiba, na wapo tunaostaafu. Nawatakia maisha mema wale wastaafu wenzangu, na nawatakia kila rakheri wale wanaowania tena.
Nichukue fursa hii kuwasihi wana MWECAU kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika serikali ya wanafunzi kwa ujasiri kabisa kwani ni haki yao kikatiba. Watu wamekuwa wakiniuluza mheshimiwa Rais unamaliza muda wako mapema sana; ukweli ni kwamba siyo mapema bali ni wakati mwafaka. Sote tunatambua kwamba ‘it doesn’t matter how a good dancer you're, you must know when to leave the stage’. And let me tell you, ‘if you are best player make sure that you struggle to keep it up or on’. Kwa mujibu wa katiba ya serikali ya wanafunzi ya chuo kikuu cha kikatioliki Mwenge toleo la 2018, kwa mamlaka niliyopewa natangaza rasmi kulivunja bunge hili tukufu la serikali ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge awamu ya 19 mwaka 2019/2020 ili kupisha shughuli za uchaguzi. Hivyo nitumie fursa hii kumtangaza rasmi mwenyekiti wa tume ya uchaguzi mkuu wa serikali ya wanafunzi awamu ya ishirini mwaka 2020/2021 Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge ndugu Jackson Magogwa.
Niwatakie kila jema katika kutimiza majukumu yenu, na huko tuendako tukawe viongozi bora kwelikweli.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU VIBARIKI VYUO VIKUU TANZANIA
MUNGU IBARIKI MWECAU
MUNGU IBARIKI MWECAUSO.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
GINAS NGOWI EMMANUEL
RAIS WA SERIKALI YA WANAFUNZI CHUO KIKUU CHA KIKATOLIKI MWENGE 2019/2020.
No comments:
Post a Comment